Mataifa ya Tanzania na Kenya yalifanikiwa kuandaa mkutano ambao utapelekea kuondolewa kwa marufuku ya bidhaa zinazoingia katika mataifa hayo mawili kutoka pande zote mbili.
Waziri wa maswala ya kigeni na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga alitangaza uamuzi huo jijini Nairobi kufuatia majadiliano kati ya rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Na kufuatia hatua hiyo Kenya itaondoa marufuku ya Unga wa ngano na Gesi inayoingia nchini humo kutoka Tanzania huku Tanzania nayo ikiondoa marufuku ya sigara na maziwa kutoka Kenya.
Kuongezea, mataifa hayo mawili yataanzisha kamati ya pamoja kuangazia maswala tofauti.
Uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara kati ya Kenya na Tanzania uliathiriwa kwa muda huku mataifa yote mawili yakiweka marufuku hizo.
Marufuku ya bidhaa kutoka Tanzania kuingia Kenya ilitokana na wasiwasi wa kiusalama na ubora wa bidhaa huku Tanzania ikijibu kwa kuweka marufuku kwa bidhaa za Kenya kama vile matairi ya gari, mafuta ya kupaka mkate na maziwa.
Tanzania pia imepiga marufuku usafirishaji wa maindi kutoka Zambia kuelekea Kenya, ambayo inakabiliwa na wakati mgumu wa ukosefu wa zao hilo muhimu.
Marufuku hizo, ikilingamishwa na idadi kubwa ya bidhaa zinazotoka na kuingia katika nchi hizo zinaweza kuathiri pakubwa biashara.
Katibu wa viwanda na uwekezaji nchini Tanzania Adolf Mkenda awali alikuwa amesema kwamba hakuna hatua zilizochukuliwa kutoka Nairobi tangu mwezi Februari na Juni wakati mataifa hayo mawili yalipokubaliana kwamba marufuku hizo ziondolewe.
No comments:
Post a Comment