Latest News

HISTORIA NA MADHARA YA LIPSTICK KWA WANAWAKE

Lipstick ni aina ya vipodozi vyenye rangi mbalimbali vinavyotumika kupaka katika midomo hasa ya wanawake ili kuongeza urembo na mvuto wao. Historia ya kupaka rangi kwenye midomo kwa kusudi la urembo inaonyesha kuwa jambo hili lilianza zamani sana na inasemekana kuwa lilianzia huko Misri.Wanawake wa Kimisri wakati huo walikuwa wanapaka rangi nyekundu kwenye midomo yao ili kuonyesha kuwa wako tayari kwa ajili ya ngono.
Maana halisi ya desturi hii ilikuwa ni kupeleka ujumbe kwa wanaume kuwa Uke wa mwanamke anayepaka rangi nyekundu mdomoni anapopata hamu ya ngono, midomo ya Uke wake inageuka kuwa na rangi nyekundu kama ile iliyopakwa kwenye midomo ya usoni.

Mwanasayansi na mtafiti wa mabadiliko ya tabia za wanadamu na maisha ya wanyama ambaye ni mwenyeji wa huko Uingereza, Desmond Morris katika kitabu chake cha “The Naked Ape (1967)” naye anaunga mkono dhana na madai hayo na anasema kuwa desturi ya wanawake kupaka rangi nyekundu kwenye midomo imetokana na wanawake kuifananisha midomo ya usoni na midomo ya uke inapovimba na kuwa na rangi nyekundu pale mwanamke anapokuwa na hamu kali ya kufanya ngono.
Kabla ya karne ya 19, kanisa Katoliki lilipinga na kuzuia matumizi ya lipstick miongoni mwa waumini wake kutokana na kuamini kuwa desturi ya upakaji wa rangi nyekundu katika midomo ya mwanamke ilikuwa na chimbuko lake kutoka katika ibada za kishetani na ufuska au umalaya. Kanisa liliendelea kufundisha hivyo kwa kipindi cha muda mrefu.
Ingawa matumizi ya rangi ya kupaka midomoni katika siku zetu inaweza kuwa na makusudi tofauti na yale ya zamani na kupendwa na wasichana au wanawake wa kisasa wanaokwenda na wakati katika urembo, lakini bado ni muhimu kuangalia athari zake kwa afya ya jamii na mwili wa mtumiaji mwenyewe.
Vipodozi hivi hutengenezwa kutokana na viambato mbalimbali na inasemekana kuwa baadhi ya viambato hivyo si salama kwa afya. Watafiti wa mambo ya afya ya jamii wanasema kuwa wanawake wengi wanaotumia rangi za kupaka midomoni wanachoangalia zaidi ni urembo na mvuto wao na wanasahau kuangalia upande wa pili wa athari zake kwa afya zao.
Katika utafiti uliofanywa huko Marekani na US Consumer Group “Campain for Safe Cosmetics” Oktoba 2007, ripoti yao iliyopewa jina la “A Poison Kiss, the Problem of Lead in Lipstick” (Busu lenye sumu) ilionyesha kuwa lipstick nyingi karibu theluthi moja, zilikuwa na madini ya ‘lead’kwa kiwango kikubwa zaidi ya kile kilicho salama kwa afya ya binadamu.
Viambato vingine vyenye madhara ambavyo vinapatikana katika rangi hizi kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari za afya ya jamii ni pamoja na Butylated Hydroxyanisole (BHA), Coal tar (petroleum) na aluminum (Lakes color).
Lakini pia ndani ya rangi za kupaka mdomoni kuna rangi ya Carmine au natural red 4, rangi inayotokana na wadudu wekundu waliokaushwa na kusagwa kama vile ‘Red Beetles’. Pamoja na rangi hii, baadhi ya vipodozi hivi pia huongezewa mafuta ya nguruwe au mafuta ya ubongo wa ng’ombe kama malighafi za kutengenezea vipodozi hivi ili viweze kulainisha midomo. Watengenezaji wengine huongeza rangi za magamba ya samaki pamoja na mazao ya mimea kama vile red beets na bizari.
Mdudu RED BEETLE anaye tumika kutengenezea Lip stick

MADHARA YA MATUMIZI YA LIPSTICK.

Wanasayansi wanaongeza kusema kuwa viambato vyenye madhara katika rangi za kupaka midomoni vinaweza kuingia mwilini au kumezwa na kusababisha athari za kiafya kama vile saratani (kansa), magonjwa ya figo, shinikizo la damu, uchovu wa mwili usiokuwa na sababu bayana, kukosekana kwa usawaziko wa kihisia (mood swing), maumivu ya kichwa, kichefuchefu, magonjwa ya ngozi, kupasuka kwa midomo (cheilitis) na magonjwa ya neva.
Matatizo mengi ya kiafya yanayosababishwa na rangi hizi, hayatokei kwa haraka na ni mara chache sana waathirika wa rangi hizi kuhusisha utokeaji wa magonjwa wanayopata na mtindo wao wa maisha wa kutumia vipodozi hivi.
Wamawake wajawazito wanaotumia vipodozi hivi, huwaweka watoto wao walioko tumboni katika hatari ya kupata magonjwa wa mtindio wa ubongo na matatizo ya akili [Utaahira]. Sumu ya lead inayopatikana katika baadhi ya vipodozi hivi hupita katika kondo la nyuma na kufika katika ubongo mchanga wa watoto walioko tumboni na kuathiri maendeleo ya ubongo na akili za mtoto, na matokeo yake ni kuzaa mtoto asiye na uwezo wa kuelewa kile anachofundishwa kwa haraka.
Wasichana na wanawake wanashauriwa kujiepusha na matumizi ya rangi hizi kwa ajili ya kulinda afya zao. Lakini kama hakuna njia nzingine zilizo salama zaidi za kukamilisha urembo wako, unashauriwa kuepuka kujilambalamba midomo pale unapokuwa umepaka rangi hizi mdomoni. Hii hupunguza kiasi cha viambato hatarishi vinavyoingia mwilini kwa njia ya kumeza, ingawa kiasi kingine kinaweza kupenya kupitia katika ngozi laini ya midomo na kuingia ndani ya damu.

No comments:

Post a Comment

NAKUJUZA Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.
Published By Gooyaabi Templates