Zoezi la upangaji wa makundi ya michuano ya Ndondo Cup 2017 limemalizika vizuri huku mwaka huu kukiwa na mapinduzi makubwa kuanzia mapema kabisa ambapo hatua ya upangaji wa makundi na hafla nzima ya uzinduzi wa hatua hiyo ilionekana mubashara kupitia kituo cha Azam TV katika channel yao ya Azam Sports HD.
Wachezaji wakichuana katika mashindano ya NDONDO CUP msimu uliopita. |
Kila kitu kilikwenda kama kilivyopangwa na kila mtu alishuhudia upangwaji wa makundi na kuridhika kwamba hakuna upendeleo wala ‘magumashi’ katika draw hiyo.
Sasa issue kubwa ikawa ni kwenye Kundi H ambalo ndio kundi la mwisho katika hatua hiyo ambapo ilishuhudiwa makundi nane yenye timu nne kwa kila kundi na kufanya jumla ya timu zote kuwa ni 32, Kundi H ndio linatajwa kuwa kundi la KIFO kutokana na kila timu mbili zilizopangwa kwenye kundi hilo kuwa na uhasama mkubwa kwenye soka.
Kauzu FC (Tandika), Faru Jeuri (Vingunguti) Sheraton (Tandika), na Miami (Vingunguti) ukiangalia kwenye Kundi hili, Kauzu na Sheraton ni timu hasimu na wapinzani wakubwa kwa upande wa Tandika timu ambazo ni majirani pale maeneo ya Tandika.
Kiongozi wa zamani wa Kauzu FC Aloyce Tembo ana story inayofanana na mtu mmoja anaitwa Peter Kenyon, wakati Roman Abrahamovic anaichukua Chelsea mtu wa kwanza kumchukua hakuwa mchezaji wala kocha, bali alikwenda Manchester United na kumchomoa Peter Kenyon ambaye wakati huo alikuwa ni mtendaji mkuu pale Man United .
Huyu mtu ndio alikuwa ubongo wa Man United, alikuwa anafanya mipango yote, laikini Abramovic alimchukua na kumhamishia Chelsea na kumpa mamlaka ya kutengeneza mipango ya Chelsea. Ni mtu huyu ndio sehemu ya mafanikio ya Atletico Madrid, watu wengi hawajui. Kenyon ndio mshauri wa karibu wa Atletico Madrid.
Sasa baada ya Sheraton kusumbuliwa sana na Kauzu kwa sababu Sheraton ni timu ya zamani sana pale maeneo ya Tandika, bada ya Kauzu kuibuka katika kipindi hiki cha Ndondo Cup, wakateka eneo la Tandika na kuwa habari ya Tandika, Tandika ni Kauzu, Kauzu ni Tandika . Sheraton walishiriki michuano ya kwanza ya Ndondo Cup lakini hawakufanya vizuri, halafu wakapotea msimu uliopita hawakushiriki kabisa.
Badae wakaangalia nguvu ya Kauzu inatoka wapi, wakagundua ni mtu wao Aloyce Tembo. Walichokifanya ni kumbeba Tembo na kumhamishia Sheraton na amewasaidia kufika hatua ya makundi ya michuano ya mwaka huu (2017) ambapo wamepangwa kundi moja. Mechi yao inatarajiwa kuisimamisha Tandika.
Ukiachana na Kauzu vs Sheraton, unakuja kukutana na Faru Jeuri na Miami, historia ya hizi timu inafanana kabisa na ile ya Liverpool na Everton. Liverpool na Everton ilikuwa timu moja lakini kutokana na kuhitilafiana katika mambo ya kiutawala kwa baadhi ya viongozi kupuuziana huku wengine kujiona ni bora kuliko wenzao ikapelekea baadhi kuamua kujiengua na kuanzisha timu yao ambayo ndio Everton.
Leo hii mechi kati ya Liverpool na Everton ni mechi ya majirani wawili ambao wanatofautishwa na mitaa tu lakini wote ni watoto wa eneo moja, sasa hii ndio story inayofanana na Faru Jeuri na Miami. Miami imetoka mgongoni kwa Faru Jeuri, baadhi ya viongozi waliokuwa Faru zamani sasa hivi wapo Miami. Hii nayo ni mechi kubwa timu hizi zitakapo kutana.
Baada ya timu za Kundi H kutajwa wakati wa zoezi la upangaji makundi, mashabiki wa timu hizo waliokuwepo kwenye hafla hiyo walikuwa wakishangilia kwa nguvu hali ambayo ilikuwa inawashangaza baadhi ya watu waliohudhuria zoezi hilo bila kujua kwamba mashabiki hao walikuwa wakishangilia derby zao.
Hii ndio orodha kamili ya makundi yote A-H ya michuano ya Ndondo Cup mwaka 2017 ambapo mechi ya ufunguzi inatarajia kupigwa Juni 17, 2017 kwenye uwanja wa Kinesi
No comments:
Post a Comment