Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania inasema imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake nchini humo.
Taarifa kutoka ikulu inasema hayo ni miongoni mwa mambo ambayo yameafikiwa katika mkutano kati ya Mwenyekiti wa Barrick Gold Corporation Prof. John L. Thornton na Rais John Magufuli.
Baada ya Mazungumzo hayo Prof. John L. Thornton amesema kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.
Mazungumzo kati ya wawili hao yalihudhuriwa na Balozi wa Canada nchini Tanzania Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi.
Rais Magufuli amesema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Prof. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu nchini humo.
No comments:
Post a Comment