Hofu imetanda kwa Watumiaji wa Matunda na Mboga za Majani Katika Viunga vya Halmashauri ya mji wa Geita baada ya kuibuka kwa Wadudu Maarufu kwa Jina la (Mdudu Mtu)wanaodaiwa kuwa na sumu kali inayoweza kusababisha kifo kwa wanyama wakiwemo Binadamu.
[Mdudu mtu] Mdudu anayeshambulia mbog za majani. |
Taarifa za kuzagaa kwa wadudu hao zilianza kutolewa na wananchi wa mitaa ya Mwatulole, Kasamwa na Nyankumbu na baadaye baadhi ya viongozi wa dini kuwatangazia waumini wao kutotumia mboga za majani baada ya wadudu hao kuonekana katika mtaa wa Mwatulole.
Mwenyekiti wa mtaa huo Charles Fikiri alisema ni kweli wadudu hao wapo, “Kwenye hili tukio la wadudu nimeshuhudia kuwaona kwenye jani la mboga mboga mpaka sasa biashara hiyo haiendeshwi vizuri kutokana na watumiaji kuhofia usalama wa afya zao.”
Wakizungumzia hali hiyo baadhi ya wananchi katika Mtaa huo, Ernestina Shamba na Yusuph Samson na wamesema mboga za majani hawatumii tena kwa hofu ya kula na kupoteza Maisha kutokana na kuenea kwa wadudu hao.
“Tunahofia kula mboga hizi kwa sababu ya hawa wadudu mtu kwa kuwa tumesikia kwa wengine wakisema wadudu hao wana madhara kwa afya za binadamu,” walisema.
Baadhi ya wafanyabiashara wa bonga za majani wameiomba serikali kufanya utafiti wa kina ili kuondoa hofu hiyo ambayo imesababisha kudorola kwa biashara mboga za majani.
“Tumeathiriwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa ndio biashara hii tunaitegemea kukidhi mahitaji ya familia zetu kwa kuwa wadudu hawa hawajawadhuru binadamu tunawaomba waendelee kutumia na tunaiomba serikali ifanye utafitijuu ya suala hili,” walisema wafanyabiashara.
Balozi wa Nyumba 10 Samson Faustine, amesema ni zaidi ya wiki moja sasa tangu wadudu hao waonekane na wamekuwa wakipendelea zaidi kwenye majani ya mboga mbalimbali pamoja na majani ya matunda kama Mpapai.
“Jana nililetewa na wananchi wakinitahadharisha kuwa wadudu hawa ni hatari ila sina hakika kama kweli wana madhara kwa afya zetu watumiaji,” alisema Faustine.
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Modest Joseph Apolnary amekiri kwenda kuwashuhudia wadudu baada ya kupigiwa simu mara kadhaa na wananchi akiarifiwa uwepo wa wadudu hao na kudai kuwa tayari amewatuma watalaamu wa kilimo na mifugo kwenda kufanya utafiti kuhusiana na wadudu hao.
“Nilipigiwa simu na wananchi kweli niliwaona wadudu hao hivyo basi tutafanya majaribio tujue kama madai hawa yana ukweli wowote ninawaomba wananchi wawe makini na uoshaji wa mboga zao,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita
Ofisa kilimo na mifugo wa Halmashauri hiyo, Paul Kamwezile amesema utafiti wa kubaini kama wadudu hao wana madhara kwa binadamu unafanyika huku akidai wadudu hao ni mzunguko wa ukuaji wa mdudu aina ya kipepeo.
“Huwakuna aina mbili kipepeo na kuna Nondo sasa watu wanashindwa kutafuta taarifa sahihi na wanadanganyana wao kwa wao,” alisema Ofisa Kilimo na Mifugo wa Halmashauri hiyo.
Aidha, Idara ya Kilimo imesema inaendelea kufanya Utafiti wa Kitalaamu kubaini ukweli wa wadudu hao na wananchi wametakiwa kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na zoezi hilo.
Na Veronica Martine, Geit
No comments:
Post a Comment