Mwanza. Pazia la Michezo ya Umitashumta litafunguliwa kesho Jumapili na kushirikisha wanamichezo 2522 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara kwenye viwanja vya Chuo ch Ualimu Butimba jijini Mwanza.
Ofisa Michezo Mkoa wa Mwanza, James Willium alisema tayari maandalizi yamekamilika na kinachosubiriwa ni kuanza kwa michezo hiyo.
Alisema kwa sasa wanaendelea kumwagia maji viwanja ili kupunguza vumbi iliyopo ili kuwarahisishia wanafunzi kucheza kwa usalama.
“Kwa ujumla maandalizi yamekamilika kwa asilimia zote, tunachofanya kwa sasa ni kuendelea kumwagilia viwanja maji ili kuondoa vumbi..lakini zaidi ni kusubiri timu kuwasili mkoani hapa,” alisema Willium.
Willium alifafanua kuwa Mikoa inatarajia kuanza kuwasili kuanzia leo Jumamosi, ambapo mashindano yataanza rasmi kesho Jumapili.
Aliwaomba wakazi wa Mwanza na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia vipaji vya watoto na kuwapa hamasa kwa maendeleo ya michezo nchini.
NMEIPENDA
ReplyDelete