Latest News

MDEE NA BULAYA KUIBUKIA MAHAKAMANI

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) amesema wanatarajia kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Bunge wa kuwasimamisha kutofanya shughuli za kibunge kwa mikutano mitatu mfululizo.

Mbunge wa Kawe Halima Mdee.


Mdee na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema), waliadhibiwa kwa makosa ya kudharau kiti cha Spika wakati bunge lilipokuwa likijadili kuhusu ripoti ya kamati. Mdee alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari. Alisema, “Nitakwenda mahakamani, wanasheria mbalimbali wameshafika, lakini tunasubiri mwanasheria mkuu wa chama ili tuanze mchakato.”

Alisema muhimili wa Mahakama uliundwa ili kusimamia haki na kutafsiri sheria. “Mahakama ni chombo pekee kilichoundwa na Katiba ili kusimamia haki, hivyo tunaamini Mahakama itatenda haki,” alisema Juni 5, mwaka huu Mdee na Bulaya walisimamishwa kutohudhuria vikao vyote vya Bunge linaloendelea mpaka mkutano ujao wa Bunge la Bajeti, Aprili mwaka 2018/19.

Hukumu hiyo baada ya kupitishwa na Bunge kwa azimio la pamoja na Spika Job Ndugai alisema hatua hiyo inalenga kuongeza nidhamu kwa wabunge wote. Mdee na mwenzake walitenda kosa Juni 2, mwaka huu wakati bunge lilipokuwa likijadili Makadilio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2017/2018. Katika kikao cha 40, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) alipewa nafasi ya kuchangia katika mjadala huo, wakati akiendelea kuchangia, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) alisimama kuomba taarifa kuhusu utaratibu naye aliruhusiwa na spika Ndugai.

Baada ya kutoa taarifa yake, Lusinde aliruhusiwa kuendelea kuchangia, kabla hajaendelea na kutoa mchango wake, Mnyika alisimama tena bila kufuata taratibu za Bunge na kuanza kusema bila ruhusa ya Spika, akidai kuwa kuna mbunge amemuita kuwa yeye ni mwizi. Spika alimtaka Mnyika akae chini ili mjadala uendelee, lakini hakufanya hivyo na ndipo Spika wa bunge walipomuagiza atolewe nje ya Ukumbi wa Bunge na kwamba kutokana na utovu wa nidhamu, asihudhurie vikao kwa siku saba.

Wakati Mnyika akitolewa, ndipo Mdee alionekana akiwakimbilia askari hao na kuvuta mashati na makoti yao ili wasiweze kufanya kama walivyokuwa wakielekezwa na spika. Wakati Mdee akifanya hivyo, Bulaya naye alionekana akisimama na kuwahimiza wabunge wa kambi ya Upinzani kutoka nje ya ukumbi huo.

No comments:

Post a Comment

NAKUJUZA Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.
Published By Gooyaabi Templates