Latest News

WACHAFUZI WA MAZINGIRA WATADHARISHWA.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa viwanda na migodi ambayo inafanya shughuli zake za uzalishaji kwa kuharibu mazingira ikiwemo utitirishaji wa kemikali kwa wananchi kwani kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa wananchi na viumbe hai vingine.

Makamu Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo kijijini Butiama mkoani Mara wakati anahutubia wananchi katika kilele cha siku ya mazingira Duniani.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema uharibifu wa mazingira ukiachiwa uendee nchini ni hatari kwa usalama wa maisha na viumbe hai, hivyo ni muhimu kwa viongozi katika ngazi zote kuchukua hatua zitakazosaidia kukabiliana na vitendo hivyo kote nchini.

Amesisitiza kuwa umefika wakati kwa viongozi kwa ushirikiano na jamii kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuokoa mifumo ya ikolojia, uhifadhi wa bioanuai, kudhibiti uchomaji miti kiholela ili kurejesha uoto wa asili ambao umeharibiwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu katika maeneo mengi nchini."Kutozingatia hifadhi ya mazingira kunaweza kusababisha kuparaganyika kwa mfumo huo na kufanya maisha yetu na ya vizazi vijavyo kuwa mashakani".
viongozi wanapaswa kuchukua hatua za kuelimisha wananchi na kuwahamasisha ili kila mtu ashiriki katika juhudi za kuwa na uchumi unaozingatia uhifadhi wa mazingira.Kuhusu wananchi kutembelea hifadhi za taifa nchini, Makamu wa Rais aipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuruhusu wananchi kutembelea hifadhi za taifa bila kiingilio na kusema mpango huo ni mzuri na unatakiwa kufanyika kila mwaka.
Amesema kuwa mkakati huo unalenga kuhamasisha wananchi ili kuwa na mahusiano rafiki na mazingira kwa kuzingatia ukweli kwamba jinsi wananchi wanapoona ndipo wanapoamini na kuelewa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Ameeleza kuwa katika kuadhimisha siku hiyo inapasa jamii kutafakari mchango wa kila sekta na kila mwananchi katika uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira January Makamba amesema Serikali imeamua kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani kijijini Butiama kama hatua ya kuenzi mchango mkubwa uliofanya na baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere katika uhifadhi wa mazingira.
Amesema baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere alifanya kwa vitendo katika kuhifadhi mazingira ambapo alianzisha msitu wake katika eneo la Butiama hivyo wananchi wote ni lazima waige mfano huo katika kulinda na kutunza mazingira.
Kwa upande wa familia ya mwalimu Nyerere wameishukuru Serikali kwa kupeleka maadhimisho hayo kijijini Butiama ikiwa ni sehemu ya kuenzi na kutambua mchango wa baba wa taifa katika uhifadhi wa mazingira nchini.
Kabla ya Kuhutubia katika Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alipanda miti katika msitu wa Mwalimu Nyerere na kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya ajali ya Ndege ya Kivita ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) uliopo katika msitu wa Muhunda katika kijiji cha Butiama mkoani Mara.

No comments:

Post a Comment

NAKUJUZA Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.
Published By Gooyaabi Templates